Social

Thursday, June 15, 2017

Uhamiaji yawashikilia wazee watano wakidaiwa kumiliki mtambo wa kughushi nyaraka




Dar es Salaam. Idara ya Uhamiaji Tanzania imewakamata wazee watano wenye umri wa kati ya miaka 55 na 64 wakituhumiwa kumiliki ofisi na mtambo wa kughushi nyaraka zikiwamo za miradi ya maendeleo ya Serikali na Mashine za Risiti za Kielektroniki (EFD).
Kamishna wa Usimamizi wa Mipaka, Samwel Magweiga amesema watu hao walikamatwa jana (Jumatano) katika ofisi yao iliyopo Barabara ya Bibi Titi Mohammed, Mtaa wa Mtendeni, wilayani Ilala.
Magweiga amesema leo Alhamisi, kuwa nyaraka wanazodaiwa kukutwa nazo ambazo ni za kughushi zilizokamatwa kwenye ofisi hiyo ni fomu za Idara ya Uhamiaji Tanzania zikiwamo za kuomba hati za kusafiri, viza, vibali vinavyowaruhusu raia wa nje kuishi nchini na kufanya kazi.
Nyingine ni vyeti vya kughushi vya ndoa na talaka kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata).
Pia, karatasi za EFD za manispaa, stakabadhi za kutoza ushuru katika halmashauri ikiwamo ya Temeke, vyeti vya vyuo vya ndani na nje ya nchi, vyeti vya kumaliza elimu ya msingi, kidato cha nne, vyeti vya elimu ya juu kikiwamo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Wanatuhumiwa kupatikana na nyaraka za uhakiki wa vyeti vya watumishi wa umma zinazoonyesha ni halali na zimetolewa na Baraza Mitihani Tanzania.
Pia, wanadaiwa kupatikana na nyaraka za kughushi za makubaliano ya miradi ya maendeleo ya Serikali, leseni za utalii za kughushi zinazotolewa na Bodi ya Utalii Tanzania, namba za utambulisho wa mlipa kodi (TIN) na nyaraka za ulipaji wa kodi  zinazotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Vyeti vya kughushi vya kuzaliwa, matangazo ya kuzaliwa ya mtoto yanayotolewa na Idara ya Msajili Mkuu wa Vizazi na Vifo, stakabadhi za halmashauri za kukusanya ushuru, vitambulisho vya mkazi, hati miliki, nyaraka za utambulisho wa utumishi wa umma wa halmashauri ya Manispaa ya Temeke, nyaraka za kupotelewa na kitu zinazotolewa na Jeshi la Polisi.
Wazee hao pia, wanadaiwa kupatikana na mihuri ya kughushi ya Benki ya Exim tawi la Mnara wa Saa na Tawi la Namanga, mhuri wa mkuu wa Shule ya Sekondari ya Jamhuri ya Dodoma, kampuni na halmashauri mbalimbali.

0 comments:

Post a Comment