Dar es Salaam. Baada ya ulinzi mkali na kuhojiwa na polisi kwa saa nne juzi, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa leo anatarajiwa kwenda tena makao makuu ya jeshi la polisi nchini kwa ajili ya mahojiano.
Lowassa alihojiwa katika ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuhusu kauli aliyotoa wakati wa futari iliyoandaliwa na mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara, Ijumaaa iliyopita
Katika futari hiyo, Lowassa anadaiwa kutoa maneno ambayo polisi wanachunguza kama yana uchochezi, alipozungumzia masheikh wa Taasisi ya Uamsho waliopo gerezani, akitaka utaratibu wa kisheria ufanyike ili kuwaachia huru.
Baada ya kuhojiwa, wakili wake Peter Kibatala ambaye pia alikuwepo katika mahojiano hayo, alisema Lowassa amejidhamini na ametakiwa kuripoti tena kwa DCI leo saa 6:00 mchana ili kujua taratibu zinazofuata.
Kibatala alisema Lowassa alihojiwa kwa tuhuma za kutoa maneno yanayoashiria uchochezi na kwamba baadaye aliandika maelezo ya onyo kuhusu kauli hiyo.
Lowassa amekuwa akikumbana na vyombo vya dola tangu aanze maisha ya siasa za upinzani.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Chadema aliihama CCM wakati joto la Uchaguzi Mkuu uliopita na baadaye kugombea urais chini ya mwamvuli wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Hafla yake na wahitimu wa vyuo vikuu mwaka jana ilizuiwa na polisi saa chache kabla ya kufanyika na ziara zake za ghafla katika maeneo ya biashara na hospitali wakati wa Uchaguzi Mkuu pia zilizuiwa na jeshi hilo.
0 comments:
Post a Comment