Social

Monday, July 31, 2017

Wabunge waliofukuzwa CUF warudi mahakamani kuzuia wateule kuapishwa Tanzania


Wabunge wanane wa viti maalumu wa CUF waliovuliwa wadhifa huo na Bunge baada ya kufukuzwa uanachama na upande wa mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba wamengua kesi mahakamani kuzuia wale walioteuliwa kuziba nafasi zao wasiapishwe.
Wabunge hao waliofukuzwa tayari wamefungua maombi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wakiiomba itoe zuio kwa Bunge kuwaapisha wabunge hao hadi kesi ya msingi waliyoifungua kupinga uamuzi wa kufukuzwa uanachama wa chama hicho itakapoamriwa.
Maombi hayo ambayo wadaiwa ni Bodi ya Wadhamini wa CUF, Tume ya Uchaguzi (NEC), katibu wa Bunge na wabunge wapya walioteuliwa na NEC, yamepangwa kusikilizwa Jumatano na Jaji Lugano Mwandambo.
Mbali na kuomba zuio dhidi ya Bunge kuwaapisha wabunge wateule, pia wanaiomba mahakama hiyo kuzuia utekelezaji wa uamuzi wa Baraza Kuu la CUF wa kuwavua uanachama.
Maombi hayo yalifunguliwa mahakamani hapo Ijumaa na wakili wa wadai hao, Peter Kibatala ikiwa ni siku moja baada ya kufungua kesi ya msingi dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa CUF, mwenyekiti wa Taifa na kaimu katibu mkuu wa chama hicho. Katika kesi hiyo namba 143 ya mwaka 2017 wadai ambao ni wabunge hao pamoja na madiwani wawili wa viti maalumu waliotimuliwa, wanaiomba mahakama hiyo ibatilishe uamuzi wa chama hicho kuwavua uanachama.
Pia, wadai hao wanaiomba mahakama hiyo itamke kuwa uamuzi huo wa kuwavua uanachama na hatimaye kupoteza nafasi zao ni batili kwa kuwa haukuzingatia kanuni za haki za msingi.
Vilevile, wanaiomba mahakama hiyo itamke kuwa mchakato wote wa kuwashughulikia kinidhamu uliohitimishwa kwa kuwavua uanachama ni batili
Wadai ambao walikuwa wabunge kabla ya kuvuliwa uanachama na kupoteza nafasi hizo ni pamoja na Miza Bakari, Savelina Mwijage, Salma Mohamed, Raisa Abdallah na Riziki Mngwali.
Wengine katika nafasi ya ubunge ni Hadija Salum Al- Qassmay, Halima Ali Mohamed na Saumu Heri Sakala wakati madiwani ni Elizabeth Magwaja na Layla Hussein.
Awali, taarifa iliyotolewa na CUF kwa Spika ikielezea kuwavua uanachama ilisema walivuliwa kutokana na makosa mbalimbali yakiwamo ya kukihujumu chama hicho.

0 comments:

Post a Comment