Social

Monday, July 31, 2017

Hatima ya Chadema kujifungia saa 48 jijini Dar es Salaam Tanzania


 Kamatakamata inayoendelea kufanywa na vyombo vya dola dhidi ya viongozi, wanachama na wafuasi wa Chadema maeneo mbalimbali nchini ni miongoni mwa masuala ambayo chama hicho kinatarajia kuyatolea azimio leo.
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, alisema Kamati Kuu ya chama hicho iliyokutana kwa siku mbili jana na juzi katika Hoteli ya Double Tree jijini hapa imejadili hali hiyo na kufikia maazimio na hatua za kuchukua.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji, Cecil Mwambe ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Kusini na mbunge wa Ndanda, mkoa wa Mtwara, Philbert Ngatunga ambaye ni katibu wa Chadema Kanda ya Kusini na Irineus Ngwatura, mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Ruvuma, hivi karibuni walikamatwa na polisi wakiwa wilayani Nyasa.
Pamoja nao, wengine waliokamatwa ni Delphin Gazia, katibu wa Chadema mkoani Ruvuma, Zubeda Sakuru ambaye ni mbunge wa Viti Maalumu; Sang'uda Manawa, katibu wa oganaizesheni na mafunzo; Cuthbert Ngwata, mwenyekiti wa Chadema wilayani Nyasa ambaye pia ni diwani wa Lipingu na Charles Makunguru, katibu wa uenezi wilayani humo.
Dk Mashinji na viongozi hao kwa pamoja walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea ambako wanakabiliwa na mashtaka mawili, la kwanza wakidaiwa wakiwa wilayani Nyasa tarehe isiyofahamika walikula njama na kutenda kosa ambalo lingeweza kusababisha uvunjifu wa amani ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Shtaka la pili wanadaiwa Julai 15 mjini Mbambabay walifanya mkusanyiko usio halali uliosababisha uvunjifu wa amani kwa jamii. Kesi hiyo itatajwa Agosti 21.
Mbali na hilo, mkoani Geita viongozi na wanachama 51 wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini walikamatwa Julai 7 na wamefunguliwa mashtaka katika Mahakama ya Wilaya ya Chato wakidaiwa kufanya mkusanyiko pasipo kuwa na kibali katika Kata ya Muganza. Wako nje kwa dhamana.
Mrema katika taarifa hiyo alisema Kamati Kuu ya chama hicho pia ilijadili na kuazimia kuhusu hali ya mwenendo wa siasa nchini na madai ya ukandamizaji wa demokrasia unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano.
Vyama vya upinzani vimekuwa vikilalamikia agizo la Rais John Magufuli la kuzuia mikutano ya hadhara isipokuwa kwa wabunge na madiwani katika maeneo yao ya majimbo na kata.
Pia, imekuwa ikielezwa kwamba katika baadhi ya maeneo mikutano ya ndani ya vyama vya siasa imekuwa ikizuiwa wahusika wakitakiwa kupata vibali kutoka polisi ili kufanya kazi hiyo ya siasa.
Mrema alisema kwamba Kamati Kuu ya chama hicho pia imejadili kuhusu kuporomoka kwa uchumi na hali ngumu ya maisha kwa wananchi.
"Taarifa kamili juu ya maazimio hayo na hatua zitakazochukuliwa na chama itatolewa kesho (leo) kwenye kikao na waandishi wa habari kitakachofanyika jijini Dar es Salaam," ilisema taarifa hiyo.

0 comments:

Post a Comment